Dar es Salaam, Tanzania – Tanlink Medical Tourism Agency kwa kushirikiana na International Eye Hospital – Dar es Salaam pamoja na Andalusia Hospital kutoka Cairo, Misri, wamezindua rasmi kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa na ubobezi wa magonjwa ya macho, ambayo itakuwa ikiendelea kuanzia tarehe 29 Juni hadi 03 Julai 2026.
Uzinduzi wa kambi hiyo umefanyika jana katika Hospitali ya International Eye Hospital iliyopo Victoria, karibu na Morocco, jijini Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kuwapatia wananchi huduma za kisasa za uchunguzi, ushauri na matibabu ya magonjwa mbalimbali ya macho kutoka kwa madaktari bingwa wenye uzoefu wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mwakilishi wa Tanlink Medical Tourism Agency alisema kuwa ushirikiano huo unaonesha dhamira ya kuendelea kuwaletea Watanzania huduma bora za afya zinazokidhi viwango vya kimataifa, huku ukitoa fursa kwa wagonjwa kupata ushauri na matibabu ya kibingwa bila ya kusafiri kwenda nje ya nchi.
“Kambi hii ni fursa muhimu kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali za macho kupata huduma za uchunguzi na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa na wabobezi. Tunawahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kufaidika na huduma hizi maalum kabla ya kambi kufungwa tarehe 03 Julai 2026,” alisema.
Huduma zinazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na uchunguzi na matibabu ya macho mekundu, uoni hafifu na kupungua uwezo wa kuona, mtoto wa jicho (Cataract), pressure ya macho (Glaucoma), magonjwa ya macho yanayosababishwa na kisukari na shinikizo la damu, magonjwa ya retina pamoja na magonjwa mengine yote ya macho.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya macho, uchunguzi wa mapema wa magonjwa ya macho ni muhimu katika kuzuia upofu na madhara mengine yanayoweza kuathiri maisha ya mtu. Hivyo, wananchi wanahimizwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kubaini changamoto za macho katika hatua za awali.
Tanlink Medical Tourism Agency imeendelea kuwahimiza wananchi wenye changamoto za macho kujisajili na kufika katika International Eye Hospital au ofisi za Tanlink Medical Tourism Agency zilizopo Haidery Plaza, Ghorofa ya Pili, Posta Mpya, Dar es Salaam, ili kupata huduma hizi muhimu za kibingwa.
Kambi hii ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya macho itaendelea hadi tarehe 03 Julai 2026 katika International Eye Hospital, Victoria karibu na Morocco, Dar es Salaam.
Kwa mawasiliano na taarifa zaidi:
📞 0654 725 770
📞 0760 003 535


