Saratani ya mapafu ni ugonjwa wa mapafu unaotokea pale seli za mapafu zinapokua na kuanza kuzaliana kwa kasi isiyo ya kawaida, na kuunda uvimbe unaoweza kuathiri sehemu nyingine za mwili.
Kwa kawaida, ugonjwa huu huanza kimyakimya — bila kuwa na dalili za dhahiri mwanzoni — jambo linalofanya utambuzi wa mapema kuwa muhimu sana.
Dalili za awali mara nyingi ni za kawaida, na watu wengi huzichanganya na magonjwa ya kawaida kama mafua, kikohozi cha muda mrefu au maambukizi ya kifua au pneumonia.
Dalili hizo ni pamoja na:
- Kikohozi kisichoisha – hasa kama kinaendelea zaidi ya wiki tatu au miezi.
- Kukohoa damu au makohozi yenye madoa ya damu.
- Kifua kubana au maumivu ya kifua yanayoongezeka wakati wa kukohoa au kupumua kwa kina.
- Kupumua kwa shida au kupumua kwa sauti ya miruzi.
- Kupungua uzito bila sababu.
- Kuchoka sana au uchovu sugu).
- Kupoteza hamu ya kula.
- Sauti kubadilika na kuwa nzito kwa muda mrefu.
- Uvimbaji wa uso au shingo ikiwa saratani imeathiri mishipa ya damu.
Kugundua saratani ya mapafu mapema huongeza nafasi ya tiba kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo basi ni muhimu kuwa makini na kujichunguza mara kwa mara au kutembelea na kupata ushauri wa kitaalamu mara tu unapohisi una dalili za saratani ya mapafu

